Na: Nassoro Rashid – Mkinga, Tanga
Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mhe. Gilbert Kalima, ametoa wito kwa wananchi wa wilaya hiyo kujitokeza kwa wingi kushiriki katika Uchaguzi Mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025, akisisitiza umuhimu wa kudumisha amani, mshikamano na utulivu katika kipindi chote cha uchaguzi.
Akizungumza katika kikao na viongozi wa dini wa Kiislamu na Kikristo, Mhe. Kalima alisema serikali inaendelea kutekeleza kalenda ya Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kwa mafanikio makubwa, huku hali ya utulivu ikiendelea kutamalaki katika Wilaya ya Mkinga.
“Tunaenda kuhitimisha kalenda ya Tume ya Uchaguzi kwa mafanikio makubwa. Ndani ya wilaya yetu amani na utulivu imetamalaki. Wapiga kura zaidi ya asilimia 80 wamejitokeza, jambo linaloonesha ushirikiano mkubwa kati ya serikali na viongozi wa dini,” alisema Mhe. Kalima.
Aidha, alibainisha kuwa kuanzia Oktoba 25, 2025, Tume itaanza kutoa matangazo rasmi katika maeneo yote ya wilaya ili kuwaelimisha na kuwakumbusha wananchi umuhimu wa kujitokeza kupiga kura.
“Tunaomba viongozi wa dini waendelee kutumia majukwaa ya ibada – Ijumaa, Jumamosi na Jumapili – kuwakumbusha waumini kwamba tarehe 29 ni siku muhimu ya uchaguzi. Wajitokeze kwa wingi bila hofu, kwani serikali imejipanga kikamilifu kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea,” aliongeza Mhe. Kalima.
Kwa upande wake, Kadhi wa Wilaya ya Mkinga, Sheikh Omari Zimbwe, alisema viongozi wa Kiislamu wamepokea kwa mikono miwili wito huo wa Mkuu wa Wilaya na wamepanga kuutumia mkutano wa Ijumaa kuhamasisha waumini kushiriki uchaguzi kwa amani.
“Sisi kama viongozi wa Kiislamu tumeupokea wito huu kwa moyo wa upendo, na tutaendelea kuwakumbusha waumini wetu wajitokeze kwa wingi siku ya uchaguzi. Tunawaomba waende kupiga kura kwa utulivu na kudumisha amani kama ilivyo desturi yetu katika Mkinga,” alisema Sheikh Zimbwe.
Naye Mchungaji Julius Clement Mtoi, Mwenyekiti wa Umoja wa Makanisa ya Kipentekoste Wilaya ya Mkinga, alisema viongozi wa Kikristo pia wameungana na serikali kuhimiza ushiriki wa wananchi katika uchaguzi kwa amani na upendo, wakitumia ibada za Jumamosi na Jumapili kama sehemu ya kuelimisha waumini.
“Tutaendelea kuhimiza waumini wetu kutumia haki yao ya kidemokrasia kwa amani na upendo. Jumamosi na Jumapili tutaendelea kuwakumbusha waumini wote wajitokeze kwa wingi kupiga kura na kudumisha utulivu kama ishara ya imani na umoja wetu,” alisema Mchungaji Mtoi.
Mhe. Kalima alihitimisha kikao hicho kwa kuwahakikishia wananchi wote kuwa serikali imejipanga vyema kuhakikisha zoezi la upigaji kura linafanyika katika mazingira ya amani, usalama na utulivu, huku akiwataka wananchi kuendelea na shughuli zao za maendeleo mara baada ya kumaliza kupiga kura.

Kasera, Tanga -HorohoroRoad
Postal Address: P O Box 6005 Tanga
Simu: +255 027-2660501
Simu: +255 684 625 299
Barua Pepe: Info@mkingadc.go.tz
Mkinga dc @ 2017