Na: Nassoro Rashid - Mkinga
Mkuu wa Wilaya ya Mkinga, Mhe. Gilbert Sylvester Kalima, amewashukuru wananchi wa Mkinga kwa ushirikiano mkubwa wanaouonesha katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya Serikali, hususan zoezi la ulipaji fidia kwa wakazi wanaopisha Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi.
Mhe. Kalima alitoa kauli hiyo mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Batilda Buriani, wakati wa hafla ya kukabidhi hundi za fidia kwa wananchi waliohamishwa kupisha hifadhi hiyo lililofanyika katika kijiji cha Mwakijembe Wilayani Mkinga.
Mkuu huyo wa Wilaya alitumia nafasi hiyo kufikisha salamu za shukrani kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuendelea kuleta maendeleo ndani ya wilaya hiyo, ikiwemo kutoa fedha za fidia shilingi Milioni 700 kwa wananchi wanaohamishwa kupisha shughuli za Serikali. Alibainisha kuwa hatua hiyo ni uthibitisho wa serikali sikivu na inayowajali wananchi wake.
Akiyataja mafanikio ya karibuni, Mhe. Kalima alisema serikali tayari imetoa fidia kwa wakazi wa Mtimbwani na Kwale kutokana na maeneo yao kuchukuliwa kwa shughuli za maendeleo. Sambamba na hilo, aliweka wazi kuwa mchakato wa fidia kwa wananchi 28 waliotoa maeneo yao kwa ajili ya shughuli za usalama mpakani upo katika hatua za mwisho.
“Naomba wananchi wetu hawa 28 waendelee kuwa na subira. Wamevuta subira kwa muda mrefu, naomba waendelee kuvuta subira kwa sababu mchakato huu upo kwenye hatua za mwisho,” alisisitiza.
Aidha, aliwahakikishia wananchi waliopisha upanuzi wa barabara ya Tanga–Horohoro kuwa serikali inautazama kwa ukaribu mchakato wa ulipaji fidia zao na muda ukifika taratibu zote zitakamilishwa. Alitoa wito kwa wananchi wote ambao uhakiki wao umekamilika kuendelea kuamini serikali yao kwa kuwa ni serikali sikivu na inayotekeleza ahadi zake.
Akizungumza katika tukio hilo, Mhe. Kalima alimpongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuahirisha ratiba zake ili kufika Mkinga kushirikiana na wananchi katika hatua muhimu ya utekelezaji wa mradi wa kitaifa.
“Kwetu sisi Mkinga tunajivunia uwepo wako, Mhe. Mkuu wa Mkoa. Kama ambavyo tumeona kupitia hotuba za viongozi waliotangulia, wananchi wamekupa imani kubwa na tunashukuru kwa namna unavyosimamia masuala ya maendeleo,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mhe. Kalima alitangaza kuanza kwa ziara maalum ndani ya Kata ya Mwakijembe wiki ijayo, ziara itakayompa nafasi ya kusikiliza moja kwa moja kero za wananchi katika kila kijiji na kufanya maamuzi ya haraka ya kukabiliana na changamoto zinazoibuliwa.

Kasera, Tanga -HorohoroRoad
Postal Address: P O Box 6005 Tanga
Simu: +255 027-2660501
Simu: +255 684 625 299
Barua Pepe: Info@mkingadc.go.tz
Mkinga dc @ 2017