Na: Nassoro Rashid - Tanga
Waziri Mkuu Majaliwa atoa wito kwa Watanzania kuimarisha lishe bora na kulinda usalama wa chakula
Oktoba 16, 2025 Watanzania wameungana na mataifa mengine duniani kuadhimisha Siku ya Chakula Duniani yakiwa na lengo kuu la kuhamasisha uzalishaji wa chakula chenye virutubisho, kuhimiza ulaji bora, kuongeza tija katika kilimo na kuhakikisha usalama wa chakula na lishe kuanzia ngazi ya kaya hadi taifa.
Lengo kubwa ni kuelimisha wananchi, hususan wale wa vijijini, kushiriki katika kufanya maamuzi sahihi kuhusu ulaji bora sambamba na kupanua matumizi ya teknolojia katika uzalishaji, usindikaji na uhifadhi wa mazao ya chakula. Hatua hizi zinakusudia kuongeza tija, kupunguza upotevu wa chakula na kupambana na changamoto za njaa, lishe duni na umasikini.
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imeongeza bajeti ya kilimo kutoka shilingi bilioni 246 hadi trilioni 1.3. Ongezeko hilo limeimarisha utafiti, upatikanaji wa pembejeo bora, huduma za ugani na upanuzi wa miundombinu ya umwagiliaji katika mabonde mbalimbali nchini.
“Matokeo ya jitihada hizi yameongeza uzalishaji wa mazao ya chakula kutoka tani milioni 18 mwaka 2020 hadi tani milioni 22 mwaka 2025. Kiwango cha utoshelevu wa chakula kimeongezeka kutoka asilimia 114 hadi 128, hali inayoonesha Tanzania sasa inazalisha chakula cha kutosha kwa matumizi ya ndani na ziada kwa kuuza nje.” alisema Mhe. Majaliwa.
Akizungumzia Mkoa wa Tanga amesema wamezalisha tani milioni 1.8 za chakula huku mahitaji yakiwa tani laki 621, jambo linalodhihirisha kuwa mkoa huo hauna upungufu wa chakula.
Aidha amesisitiza kuwa Sekta ya mifugo imeendelea kukua kwa kasi ambapo mwaka 2025 idadi ya ng’ombe imefikia milioni 39.2, mbuzi milioni 28.6, kondoo milioni 9.7 na kuku milioni 108, uzalishaji wa nyama umefikia tani 963,856 na maziwa lita bilioni 3.97 na upatikanaji wa mayai umefikia milioni 7, ishara kwamba sekta hii inachangia kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa chakula chenye protini bora.
"Vilevile, sekta ya uvuvi imeongezeka uzalishaji hadi tani 522,788, ikiwemo tani 132,245 za mazao ya ukuzaji viumbe hai vyenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 315. Hii inaonesha mafanikio ya uwekezaji katika ufugaji wa samaki na mabwawa ya kisasa". Aliongeza Mhe. Majaliwa.
Pia amesema hali ya lishe nchini imeendelea kuimarika ambapo kiwango cha udumavu kimepungua kutoka 34% mwaka 2015 hadi 30% mwaka 2022. Ukondefu kwa watoto chini ya miaka 5 umeshuka hadi asilimia 3.3. Mkoa wa Tanga umeonesha mfano bora kwa kupunguza udumavu kutoka asilimia 34 mwaka 2018 hadi 28 mwaka 2025, kutokana na utekelezaji mzuri wa sera na ushirikishwaji wa jamii.
Hata hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa wananchi kuepuka ulaji usio sahihi unaosababisha unene kupita kiasi na magonjwa yasiyoambukiza kama presha na kisukari, akihimiza kufanya mazoezi mara kwa mara na kula kwa kufuata kanuni za lishe bora.
Maadhimisho haya ni fursa ya kuenzi mafanikio, kuimarisha umoja na kuhamasisha juhudi za kuhakikisha kila kaya inapata chakula cha kutosha na chenye ubora. Tukidumisha uzalishaji endelevu na lishe bora, Tanzania itaendelea kuwa na afya imara, uchumi thabiti na mustakabali bora kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Kasera, Tanga -HorohoroRoad
Postal Address: P O Box 6005 Tanga
Simu: +255 027-2660501
Simu: +255 684 625 299
Barua Pepe: Info@mkingadc.go.tz
Mkinga dc @ 2017