Na: Nassoro Rashid – Mkinga
Serikali kupitia Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga imezindua rasmi zoezi la ulipaji fidia kwa wananchi wanaohamishwa kupisha eneo la Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi, katika Kitongoji cha Kimuuni, Kijiji cha Mkota, Kata ya Mwakijembe, Wilaya ya Mkinga. Zoezi hilo limezinduliwa na Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Mhe. Balozi Dkt. Batilda Salha Buriani, ambaye amekabidhi hundi kwa wanufaika na kusisitiza kuwa Serikali imejipanga kuhakikisha fidia inalipwa kwa haki, uwazi na kwa kufuata sheria.
Akihutubia mamia ya wananchi waliojitokeza, Dkt. Batilda alibainisha kuwa Serikali imefanya mageuzi makubwa ya kiutawala na kiutendaji ili kutatua migogoro ya muda mrefu baina ya wananchi na maeneo yaliyohifadhiwa.
Alisema jitihada za kamati ya kisekta zimesaidia kukamilisha tathmini, na maeneo yaliyokuwa na utata yamepitiwa upya kwa ushirikiano wa ofisi zote za ardhi mkoani, TANAPA, TFS, na vyombo vingine vya uhifadhi ambapo jumla ya shilingi Milioni 700 ilibainishwa kuwa stahiki ya fidia kwa Wananchi 115.
"Serikali imeamua kuwahakikishia wananchi haki yao. Waliothaminiwa 115 wamelipwa, lakini tunawataka wataalam kuwarudia wale 25 ambao hawakukamilisha nyaraka ili na wao wapate haki yao. Hili zoezi ni la wananchi wote,” alisema RC Batilda.
Akizungumza kuhusu makazi mapya na mpango wa uhamisho Dkt. Batilda alieleza kuwa Serikali tayari imebainisha eneo kubwa ndani ya pori tengefu lenye zaidi ya hekta 454, linalogusa Korogwe, Lushoto na maeneo mengine, ambalo litatumika kwa mpango rasmi wa makazi mapya. Alisisitiza kuwa mpango wa matumizi bora ya ardhi utahakikisha wananchi wanaohamia hawapotezi fursa walizokuwa nazo hapo awali.
Aidha, alizitaka taasisi husika kukamilisha mpango wa makazi kwa siku 60, ili shughuli za uhifadhi ziendelee, ikiwemo uanzishwaji wa lango jipya la hifadhi upande wa Mkinga kwa ajili ya kuboresha utalii.
Katika kupambana na Wanyamapori Wakali Mhe. Batilda amesema Serikali inatekeleza mikakati madhubuti ya kukabiliana na tembo wavamizi, ikiwemo matumizi ya ndege maalum za kufukuza tembo, pamoja na kuanzisha miradi ya ufugaji nyuki katika maeneo ya mipaka ya hifadhi.
“Tembo hawavuki maeneo yenye mzinga wa nyuki. Tunaiomba TANAPA kuanzisha miradi ya kijamii na kiuchumi, hasa ufugaji wa nyuki, ili kulinda mazao na kuleta kipato kwa wananchi,” alisisitiza.
Amesema fidia zote zinalipwa kwa kutumia hundi za benki ili kuondoa mianya ya wizi na makosa ya kimfumo. Aliitaka NMB na CRDB kutoa ushirikiano kwa wananchi na kutoa elimu ya matumizi sahihi ya fedha wanazopokea.
“Usikimbilie kutumia fedha bila mpango. Kaeni, shaurianeni, ombeni Mungu. Fedha hizi ziwe mbegu ya kubadilisha maisha yenu,” alihimiza.
RC Batilda alisema kuimarika kwa hifadhi kutafungua milango kwa wawekezaji, hususan hoteli, kambi za watalii na biashara za utalii wa kuona. Alibainisha kuwa watalii kutoka Zanzibar wanaweza kufika Mkomazi kwa urahisi kutokana na uwepo wa ndege tatu zinazokuja Tanga kila siku.
“Mkinga inaenda kuwa mlango mpya wa utalii nchini. Tuchangamkie fursa hizi,” alisema.
Katika hatua nyingine, Mkuu wa Mkoa aliwasisitiza wananchi kudumisha amani na mshikamano, hususan katika kipindi hiki ambacho taifa linapitia hatua muhimu za maendeleo na utekelezaji wa miradi ya kimkakati. Alisema kuwa amani ndiyo nguzo ya ustawi wa kijamii na kiuchumi, hivyo kila mwananchi ana wajibu wa kuilinda na kuithamini.
Aidha, aliwaasa vijana kuwa mstari wa mbele katika kuitetea amani ya nchi, kuepuka ushawishi wa maneno ya uchochezi, matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii na vitendo vinavyoweza kuvuruga utulivu wa jamii.
“Ninawaomba vijana wetu, mnalolinda leo ndilo litakalowajenga kesho. Msimamo wenu ni muhimu. Linda amani, dumisha mshikamano. Bila amani hakuna maendeleo, na bila umoja hakuna nguvu ya kuijenga Mkinga na Tanzania kwa ujumla,” alisisitiza.
Akihitimisha hotuba yake, Mkuu wa Mkoa aliwahakikishia wananchi kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kusimamia maendeleo, usalama na ustawi wa wananchi wote wa Mkoa wa Tanga.

Kasera, Tanga -HorohoroRoad
Postal Address: P O Box 6005 Tanga
Simu: +255 027-2660501
Simu: +255 684 625 299
Barua Pepe: Info@mkingadc.go.tz
Mkinga dc @ 2017